Category : Social | Sub Category : Education Posted on 2023-06-27 16:46:14
Ili kupunguza mifarakano inayopeleka kuvunjika kwa ndoa,Wanandoa
wamekumbushwa kuvumiliana kulingana na mapungufu yao kwa sababu hakuna mtu
aliyokamilika asilimia mia kuwa na vigezo vyote wanavyotarajia.
Bi. Leyla Abubakari ambaye ni Mwanasaikolojia wa masuala ya malezi
akizungumza na Radio Nuur fm katika Kipindi cha Mseto kinachorushwa na kituo
hiki Jumatatu hadi alhamisi amesema siri ya kuishi na mtu wa jinsia tofauti
(mume/mke) ni kumuangalia kwa jicho la wema katika mabaya yake na kumrekebisha
kwa kauli nzuri.
“Akifanya kitu ambacho kinakukera au amekosea usimuangalie kwa jicho lake
la tabia mbaya bali kubali kuwa ni mapungufu yake na unatakiwa umvumilie na
kumuelekeza kwa kutumia kauli nzuri ambazo hazitamkera na wala kuona kama
amedharauliwa”,amesema Bi Leyla.
Aidha Mwanasaikolojia huyo ambaye pia Mwalimu amesema kuwa wanandoa
wajifunze kuacha mazoea ya kutoa siri zao nje kitu ambacho kinaweza kupoteza
amani ndani ya ndoa zao.
“Kuna tabia ya wanandoa kuona ni kawaida kushitaki kwa ndugu,jamaa au
marafiki kuhusu matatizo yenu ya ndani jambo ambalo huzaa kuzarauliwa au
kutendwa kutokana na kutokuficha mambo yenu ya ndani ambayo yalistahili
kumalizwa na wana ndoa husika bila kutafuta ushauri wa nje”,Amesema Bi. Leyla.
Utafiti unaonesha wanandoa
wengi wamekuwa wakiingia kwenye ndoa huku wakiamini wale wanaokuwa nao
wamekamilika na watakuwa vile ambavyo wao wanataka kitu ambacho sio sahihi
kwani hujisahau kuwa wamekulia katika malezi ya familia tofauti.